Tuesday, November 27

Raisi Magufuli atoa onyo kali kwa upinzani Tanzania

Rais wa Tanzania John Magufuli ametuma salamu kwa wapinzani Tanzania akiwaonya kuishia jela iwapo 'hawataheshimu sheria'.

Magufuli amempa salamu hizo waziri mkuu wa zamani Edward Lowassa ambaye sasa ni kiongozi wa chama cha upinzani Chadema.

Magufuli na Lowassa walikutana leo Jumanne Novemba 27 katika ufunguzi wa maktaba ya kisasa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

"Ninakupongeza sana (Lowassa). Hii ndiyo Tanzania mpya tunayoitaka. Vyama vyetu visiwe chanzo cha kututenganisha bali viwe chachu ya kuleta maendeleo," amesema Magufuli na kuongeza: "Hii ndio Tanzania mpya tunayoitaka, "Nimeona hili nilizungumze kwa heshima kubwa, Mzee Lowassa ili wale unaowaongoza kule, uende ukawashauri, otherwise (lasivyo) wataishia magereza ili wakajifunze namna ya kuheshimu sheria za Watanzania."

Magufuli amemwagia sifa Lowassa kuwa licha ya kumshinda kwenye uchaguzi wa mwaka 2015 ameendelea kuwa mtulivu. 

Viongozi kadhaa wa upinzani Tanzania wakiwemo wa chama cha Chadema ambacho Lowassa ni mjumbe wa kamati kuu wanashtakiwa mahakamani kwa kwa kesi mbalimbali.

Wiki iliyopita, mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alifutiwa dhamana pamoja na mbunge wa Tarime
Mjini, Esther Matiko kutokana na kukiuka masharti ya dhamana katika kesi inayowakabili ya kufanya mikusanyiko kinyume cha sheria.

Mashtaka mengine yanayowakabili viongozi wa upinzani ni uchochezi na kutoa maneno yasiyofaa dhidi ya Rais.

Misaada ya Uchina

Katika hafla hiyo Magufuli pia aliwasifu Wachina kuwa wanatoa misaada isiyokuwa na masharti.
"China ni marafiki wazuri wametoa zaidi ya Bilioni 90 fedha za walipa kodi wao bila masharti, maana wengine wangetoa masharti. Naomba Balozi ufikishe asante zetu kwa Rais wenu, asante kwa wananchi wa China pia."

Hivi karibuni Tanzania imekuwa ikipitia wakati mgumu kwenye suala la masharti ya misaada na mikopo.

Benki ya Dunia imezuia mkopo wa dola milioni 300 wa kuboresha elimu ya sekondari ikitaka serikali ya Tanzania ibadili sera yake ya kuzuia wanafunzi wa kike kuendelea na masomo baada ya kujifungua.

Serikali ya Denmark imezuia msaada wa dola milioni 10 baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda kutoa kauli kali dhidi ya wapenzi wa jinsia moja.



No comments:

Post a Comment